image

Uhuru kaa kidete!

Sifichi Nuhu sifichi, bora niseme ukweli,
Mbivu imekuwa mbichi, na haramu ni halali,
Kenya sasa iko uchi, wezi wametufidhuli, 
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

Wizi umekuwa mila, bunge letu limeoza,
Viongozi wenye hila, wote tutawachunguza,
Kisha wapelekwe jela, waache kutuchagaza,
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

Mafisadi wamejaa, katika mabunge yetu,
Kimeshazidi kinyaa, tuwakanyeni wenzetu,
Ni bora kuwakataa, walaji wa pesa zetu,
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

Nakushauri Uhuru, ni bora ukae ange,
Hebu piga haidhuru, wafukuze viberenge,
Maji mekuwa gururu, washike mamburukenge,
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

Umejaa ukabila, katika kila ofisi,
Watu mekuwa juhula, Kenya nchi ya nuhusi,
Kila siku wanakula, tena bila wasiwasi,
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

Wameanza kutajana, katika zao sakata,
Sio juzi sio jana, ndoa imeshatokota,
Mtawajua bayana, kwa kiburi na kunyeta,
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

Nimefika kaditama, mwisho wa shairi langu,
Ninakuomba Karima, iokoe nchi yangu,
Wape waizi huruma, waache ubangubangu,
Uhuru kaa kidete, nchi inaporomoka;

©Utunzi wa:
Nuhu Zubeir Bakari
“Al-Ustadh Pasua”

@Nariari Auliver™
©2016

Advertisements