Kaguta kuwa mpole!

Ewe Rais Kaguta, punguza wako unyama,
Nakuona unanyeta, unapenda madhuluma,
Kura unapotafuta, wenzio wape heshima,
Kaguta kuwa mpole, usidhulumu wenzio!

Juzi nimekushangaa, kwenye yako michakato,
Fujo imezagazaa, metembeza mkong’oto,
Kizza umemsumbua, wacha simpige ngoto,
Kaguta kuwa mpole, usidhulumu wenzio!

Simuonee Besigye, Waganda wanalalama,
Mbona wamtesa yeye, simfanyie unyama,
Wacha chako kiseyeye, Kaguta fanya huruma,
Kaguta kuwa mpole, usidhulumu wenzio!

Usitumie Polisi, kumsumbua mwenzako,
Nilipo mimi nahisi, umeuona mjiko,
Yoweri una nuhusi, mtu feki mwenye mbeko,
Kaguta kuwa mpole, usidhulumu wenzio!

Kizza anapotembea, kwenye jiji Kampala,
Koma kumzoazoa, kum’beba kwa machela,
Wacha kumsongonyoa, Kizza kumpiga ngwala,
Kaguta kuwa mpole, usidhulumu wenzio!

Hapa nafunga suhufa, Kamanda ninaondoka,
Nasambaluka mshefa, na bendera nimeshika,
Yoweri hauna sifa, kwa hilo umeanguka,
Kaguta kuwa mpole, usidhulumu wenzio!

©Utunzi wa:
Nuhu Zubeir Bakari,
“Al-Ustadh Pasua”

image

@Nariari Auliver™
©2016

Advertisements